CHANGA MOTO HUDUMA YA AFYA ILEMELA, SERIKALI YAWAONYA WAHUDUMU
Serikali yawaonya wahudumu wa afya Ilemela
SERIKALI kupitia Idara ya Afya,
Wilaya ya Ilemela, Mwanza imewaonya wahudumu wa afya wanaofanya kazi kwa mazoea
badala ya kutumia weledi wao katika kuihudumia jamii ili kuepusha vifo visivyo
vya lazima.
Onyo hilo lilitolewa juzi jijini
Mwanza na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Desderius Polle wakati akifungua
semina iliyoandaliwa na Chuo cha Mafunzo na Maendeleo (MC TCDC) chini ya
ufadhili wa hospitali ya Aga Khan, kupitia mradi wa Joining Hands Initiative
(JHI).
Semina hiyo imewashirikisha wahudumu
mbalimbali wa afya kutoka kata mbili za Pamba na Butimba jijini hapa.
Polle ambaye pia ni Ofisa Afya wa
Ilemela, alieleza kuwa wahudumu wa afya ni muhimu katika ustawi wa jamii na
maendeleo ya taifa, hivyo ni vema wataalamu hao watimize wajibu ipasavyo.
Awali mkufunzi wa mafunzo hayo,
Joram Masesa aliwasihi wauguzi wote kutekeleza vema majukumu yao ili kuokoa
uhai wa mama na mtoto.
Kwa mujibu wa Masesa, vifo vya
wanawake vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga chini ya miaka mitano
lazima vitokomezwe ili kujenga jamii salama.
0 comments:
Post a Comment